Wizara ya Mambo ya Ndani ya Yemen imetoa tamko na kuthibitisha habari ya kuuawa rais wa zamani wa nchi hiyo, Ali Abdullah Saleh.
Leo jioni Wizara ya Mambo ya Ndani ya Yemen imesema katika tamko lake kwamba Ali Abdullah Saleh, ameuawa.
Yahya al Mahdi, mkuu wa idara ya itikadi
katika jeshi la Yemen naye amethibitisha habari ya kuuawa Ali Abdullah
Sale na kusema kuwa, rais huyo wa Yemen ameuawa wakati alipokuwa
akikimbia kutoka mjini San'a kuelekea Ma'rib.
Amesema, vikosi vya usalama vya Yemen
leo Jumatatu viligundua njia aliyokuwa anatumia Ali Abdullah Saleh
kutoka eneo moja kwenda eneo jingine na walipata taarifa za
kiitelijinsia za namna wafuasi wake walivyokuwa wanapanga kumtorosha
San'a na kumkimbiza mafichoni Ma'rib.
Mkuu huyo wa idara ya itikadi ya jeshi
la Yemen ameongeza kuwa, maafisa usalama wa nchi hiyo walianza
operesheni ya kumtia mbaroni Ali Abdullah Saleh mara alipofika katika
eneo la Sanhan. Hata hivyo walinzi wake hawakuwaruhusu maafisa usalama
wa Yemen kumtia mbaroni na hapo ukatokea ufyatulianaji risasi baina ya
pande mbili ambao umeishia kwenye kuuawa Ali Abdullah Saleh na viongozi
wengine wa ngazi za juu wa chama chake.
Habari ya kuuawa Ali Abdullah Saleh
imethibitishwa pia na picha kadhaa pamoja na mkanda wa video ulioenea
katika mitandao ya kijamii.
Kuanzia siku chache zilizopita, mji mkuu
wa Yemen, San'a umekuwa ukishuhudia mapigano baina ya makundi yenye
silaha ya Ali Abdullah Saleh na jeshi na kamati za kujitolea za wananchi
zenye mfungamano na harakati ya Answarullah.
Taarifa zinasema kuwa, fitna ya hivi
sasa iliyoanzishwa na rais wa zamani wa Yemen dhidi ya harakati ya
Answarullah na uhusiano wa karibu wa Ali Abdullah Saleh na Saudi Arabia
ni katika njama zilizokuwa zinaendeshwa na Umoja wa Falme za Kiarabu
(Imarati) za kutaka kuurudisha madarakani ukoo wa Ali Abdullah Saleh
nchini Yemen.
No comments:
Post a Comment