Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ameapishwa
kuiongoza nchi hiyo kwa muhula wa pili wa miaka mitano mjini Nairobi leo
katika sherehe iliyohudhuriwa na maelfu ya wafuasi wake na viongozi
kadhaa wa nchi za Afrika.
Rais Kenyatta amekula kiapo katika Uwanja wa Kasarani mjini
Nairobi kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26
ambao ulisusiwa na kinara wa upinzani Raila Odinga kwa madai kuwa
haukuwa huru na wa haki. Mahakama ya Kilele Kenya ilibatilisha uchaguzi
uliokuwa umefanyika Agosti nane kwa msingi kuwa kulikuwepo na dosari.
Kati ya viongozi waliohudhuria sherehe hizo ni Waziri Mkuu wa
Ethiopia Hailemariam Desalegn, Marais Paul Kagame wa Rwanda, Mohamed
Abdullahi Mohamed wa Somalia, Salva Kiir wa Sudan Kusini, Ian Khama wa
Botswana Yoweri Museveni wa Uganda, Omar Bongo wa Gabon, Egar Lungu wa
Zambia, Ismaïl Omar Guelleh wa Djibouti,
na Hage Geingob wa Namibia. Tanzania imewakilishwa na Makamu wa Rais
Samia Suluhu baada ya Rais John Magufuli kukosa kuhudhuria kama
ilivyotarajiwa. Katika hotuba yake, Rais Kenyatta ametangaza kwamba
Mwafrika yeyote atapewa viza akifika katika kiingilio chochote mpakani
au viwanja vya ndege Kenya.
Aidha Kenyatta amesema ana malengo mawili katika muhula wake wa
mwisho. Kwanza kuimarisha uwiano na umoja miongoni mwa Wakenya.
Ameongeza kuwa ameanza kuwasiliana na viongozi wote na kueleza nia yake
ya kuendeleza umoja. Halikadhalika amesema lengo la pili ni kuhakikisha
huduma ya afya inawafikia Wakenya 100%. Naibu wa Rais William Ruto pia
ameapishwa katika sherehe hiyo.
Katika upande mwingine polisi mjini
Nairobi waliliazimka kutumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi
wa Raila Odinga waliokuwa wanakutana katika uwanja wa Jacaranda katika
mtaa wa Embakasi walikokuwa wamekusanyika kuwaomboleza waliouawa katika ghasia za baada ya uchaguzi.
No comments:
Post a Comment