Imeelezwa kuwa, umasikini na kipato cha chini
cha baadhi ya familia nchini Tanzania ndicho chanzo cha mimba za
utotoni katika jamii ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti
katika warsha ya siku moja ya kutambulisha mradi na shirika hilo kwa
wadau iliyofanyika mkoani Dodoma. Kwa mujibu wa shirika hilo, utafiti
uliofanywa na shirika hilo kwa kusaidiana na mashirika mengine, umebaini
kwamba, umasikini wa familia husababisha familia zenye maisha magumu
kupambana kwa bidii kutafuta chakula na mavazi ya watoto wao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Jukwaa
la Utu wa Mtoto ameeleza kuwa, utafiti wa Demografia ya Afya Tanzania
wa 2016 (TDHS) unaonesha kwamba, asilimia 36 ya wasichana wa umri wa
kati ya miaka 20-24 waliolewa kabla ya kufikia miaka 18.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, kumekuweko na kampeni ya kimataifa ya kukabiliana na ndoa za utotoni hasa barani Afrika.
Mwezi uliopita nchi ya Senegal ilikuwa
mwenyeji wa mkutano uliokuwa na lengo la kuongeza hatua za kutokomeza
ndoa za utotoni katika nchi za Afrika Magharibi na Kati. Inaelezwa kuwa,
wazazi ambao hali zao ni duni kimaisha, mara nyingi huwaozesha watoto
wao mapema ili kupunguza mzigo wa ulezi, wakati huo huo, baadhi ya mila
na desturi zinatajwa kuwa nazo zina mchango katika hilo.
No comments:
Post a Comment