Waziri Mkuu wa Korea Kusini anayekaimu nafasi
ya rais, amelitaka jeshi na vikosi vya nchi hiyo kujiweka tayari
kutokana na kile alichokisema kuwa ni kushadidi kwa harakati za kijeshi
za Pyongyang.
Hwang Kyo-ahn ameyasema hayo Alkhamis ya leo katika kikao cha
Baraza la Mawaziri la Korea Kusini kufuatia kuenea kwa habari
zinazohusiana na uwezekano wa Korea Kaskazini kufanya jaribio la sita la
silaha ya nyuklia hivi karibuni. Kufuatia hali hiyo Hwang Kyo-ahn
ametoa amri kwa jeshi la nchi yake kujiweka tayari kwa ajili ya
kukabiliana na hatua yoyote ya kijeshi na harakati za Korea Kaskazini.
Kadhalika Waziri Mkuu wa Korea Kusini amelitaka jeshi la nchi hiyo
kufuatilia kwa karibu mabadiliko na harakati zote za Pyongyang. Mgogoro
katika eneo la Peninsula ya Korea ulishadidi baada ya Rais Donald Trum
wa Marekani na makamu wake wa rais, Mike Pence kutoa matamshi ya vitisho
kuilenga Pyongyang, vitisho ambavyo vilienda sambamba na kutumwa kwa
meli tatu za kijeshi zinazobeba ndege za kivita karibu na pwani ya Korea
Kaskazini.
Hatua hiyo ya Marekani ilitajwa na Korea Kaskazini kuwa, ya kichokozi
na inayohatarisha usalama na amani ya peninsula hiyo. Mbali na hayo ni
kwamba Korea Kaskazini imesisitiza mara kadhaa kwamba, madamu Marekani
na waitifaki wake zitaendelea kutishia usalama wake, basi nayo itazidi
kuimarisha uwezo wake wa kijeshi kukabiliana na chokochoko za adui.
No comments:
Post a Comment