Umoja wa Mataifa umeutaka muungano wa kijeshi wa Saudi Arabia usishambulie kwa mabomu bandari ya kistaratejia ya Yemen.
Jamie McGoldrick, Mshirikishi wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja
wa Mataifa nchini Yemen ametahadharisha kuwa, iwapo Bandari ya
al-Hudaydah iliyopo katika Bahari Nyekundu itashambuliwa kwa mabomu na
Saudia, basi yumkini idadi kubwa ya raia wa Yemen wakatumbukia katika
mgogoro mkubwa wa kibinadamu.
Katika kikao na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Jordan, Amman
hii leo, afisa huyo wa UN amefafanua kuwa: "Bandari ya al-Hudayda ni
kituo nyeti kwa raia wa Yemen, hatuoni iwapo kuna haja ya eneo hilo la
kistaratajia kushambuliwa na muungano wa kijeshi wa Saudia. Muungano huo
unafaa kulipa uzito na umuhimu suala la kibinadamu unapokuwa katika
kampeni na operesheni zake. Iwapo bandari hiyo itashambuliwa, sisi
pamoja na asasi zingine za kufikisha misaada ya kibinadamu hatutaweza
kufikisha chakula, dawa na mahitaji mengine ya msingi kwa raia wa
Yemen."
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Bandari ya al-Hudaydah ndiyo bandari
muhimu zaidi ya Yemen ambapo karibu asilimia 80 ya shehena za chakula na
dawa zinazofikishwa kwa wananchi, hupitishwa kupitia bandari hiyo.
Hii ni katika hali ambayo, wananchi wa Yemen hapo jana walikusanyika
mbele ya ofisi ya Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa nchi hiyo Sana'a
kulaani kufungwa Bandari ya al-Hudaydah sambamba na kukosoa mauaji ya
kikatili dhidi ya watu wa taifa hilo, yanayofanywa na muungano vamizi wa
kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, tangu Machi mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment