Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan
amemuhakikishia Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq kwamba, watu waliohusika
na kuwavunjia heshima shakhsia muhimu wa Iraq, wametiwa mbaroni na
kwamba watafikiishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Ayman Safadi ameyasema hayo katika
mazungumzo ya simu na waziri mwenzake wa Iraq, Ibrahim al-Jaafari
ambapo sambamba na kusisitizia umuhimu wa kuimarishwa mahusiano baina ya
Aman na Baghdad, amesema kuwa Jordan inalaani aina yoyote ya uvunjiwaji
heshima taifa la Iraq.
Kabla ya hapo Ahmad Jamal, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq
alikosoa vikali kimya cha serikali ya Jordan juu ya kitendo cha baadhi
ya raia wa nchi hiyo cha kuwavunjia heshima baadhi ya shakhsia muhimu wa
Iraq ikiwemo kuichoma moto picha za maraajii wakubwa wa nchi hiyo.
Alisema kuwa, kitendo hicho ndicho kiliifanya serikali ya Baghdad
kumwita balozi mdogo wa Jordan nchini Iraq, kwenda kujieleza katika
Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo.
Jumamosi iliyopita, mbunge mmoja wa Iraq alitangaza kuwa, kundi moja
la raia wa Jordan liliivunjia heshima picha za maraajii wa kidini na
shakhsia wengine wa kisiasa akiwemo Nouri al-Maliki, Makamu wa Rais wa
Iraq.
No comments:
Post a Comment