Thursday, April 20, 2017

SERA ZA MAREKANI KATIKA MASHARIKI YA KATI NI KUENEZA HOFU NA VITISHO DHIDI YA IRAN

James Mattis, Waziri wa Ulinzi wa Marekani amesema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Riyadh Saudi Arabia baada ya kukutana na mwenyeji wake kwamba, timu ya Rais Donald Trump inaandaa mikakati ya kuidhibiti na kuikwamisha Iran kupitia njia ya kuimarisha uratibu na Saudi Arabia na waitifaki wengine wa Marekani.
Jenerali Mattis amedai kwamba, Iran imekuwa ikivuruga amani na uthabiti katika Mashariki ya Kati hivyo kuna haja ya kuzuia satwa na ushawishi wa taifa hili ili ipatikane njia ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Yemen kupitia mazungumzo kwa upataishi wa Umoja wa Mataifa. Kwa hakika matamshi haya ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani si jambo jipya. Viongozi wa Marekani bila kujali ni wa chama cha Democrats au cha Repulican wamekuwa wakitumia lugha hizo za vitisho tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipopata ushindi na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ulipokuja na kukata mikono ya Marekani hapa nchini.
Kwa muktadha huo, uadui wa madola yanayotumia mabavu ulimwenguni hususan Marekani kwa taifa taifa la Iran ni jambo lisilo na shaka hata kidogo. Hii inatokana na kuwa, uadui wao uliendelea kushuhudiwa katika kipindi chote ambacho serikali mbalimbali na zenye utashi tofauti zilipoingia madarakani nchini Marekani.
Safari ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani nchini Saudia
Pamoja na hayo, inaonekana kuwa, lengo la viongozi wa Marekani katika kipindi hiki la kutumia lugha hizi za vitisho ni kutoa ishara ya kuweko mabadiliko ya kimsingi katika sera za Marekani katika kukabiliana na Iran. Hivi sasa siasa za Marekani dhidi ya Iran kwa namna fulani zinaonekana kuipa Saudi Arabia baadhi ya majukumu. Kiasi kwamba, akitoa natija jumla ya mazungumzo yake huko Riyadh, Waziri wa Ulinzi wa Marekani amesema kuwa, Washington imefikia natija na Riyadh kuhusiana na jambo hilo.  Mattis amesema: Kwa hakika sisi tunapaswa kufanya kitu na kuimarisha muqawama wa Saudia mbele ya miamala ya Iran. Kama ambavyo tunafanya kazi tukiwa washirika, tunapaswa kuchukua hatua ambazo zitakufanyeni nyinyi viongozi wa Saudia na jeshi lenu muwe na utendaji mzuri zaidi.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani ameyatoa matamshi na madai haya mjini Riyadh katika hali ambayo, kila mahala ambako kuna matatizo katika Mashariki ya Kati na popote pale ambako kunafukuta moto wa vita kuanzia Asia mpaka Ulaya na Afrika mpaka Amerika ya Latini basi kunashuhudiwa mkono wa Marekani na waitifaki wake.
Aidha stratejia ya Marekani katika Mashariki ya Kati inaeleweka wazi. Stratejia hiyo haina tofauti sana na duru zilizopita za uongozi nchini Marekani kabla ya Rais wa sasa wa nchi hiyo Donald Trump. Marekani ingali inawategemea watawala wa nchi za Kiarabu wa eneo hili katika uuzaji silaha zake kwa kisingizio cha kukabilia na vitisho ambavyo Marekani yenyewe imevipandikiza. Utawala wa Aal Saud nao ukitumia mbinu ya kale umekuwa ukinunua silaha nyingi kwa kutumia fedha za mafuta ikiwa na lengo la kununua muda zaidi kwa utawala wake unaotetereka na kulegalega.
Katika uwanja huo, himaya ya Marekani kwa uvamizi wa Saudia katika vita vya Yemen ni jambo muhimu, kwani kivitendo siasa za chokochoko za Saudia katika vita hivyo na vile vile katika kuyaunga mkono makundi ya kigaidi huko Syria na Iraq zimeshindwa na kugonga mwamba. Njia pekee iliyobakia kwa Aal Saud ni kutoa upendeleo kwa Marekani usio na masharti yoyote. Hata hivyo inawezekana kuyatazama matamshi haya ya Mattis katika engo nyingine. Waziri huyo wa Ulinzi wa Marekani anasema kuwa, Washington na washirika wake wanataka kuikwamisha Iran.
Matamshi haya kwa namna fulani yanaweza kuwa yana lengo la kupima radiamali ya Iran mkabala na lugha za vitisho za Marekani. Kwani viongozi wa White House wanatambua vyema msimamo wa Iran kuhusiana na jambo hilo. 
Ayatullah Ali Khamenei, alipokuna na makamanda wa jeshi kwa mnasaba wa Siku ya Jeshi nchini Iran
Akihutubia Jumatano ya jana kwa mnasaba wa Siku ya Jeshi hapa nchini, wakati alipokutana na kundi la makamanda wa jeshi, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema kuwa, moja ya nukta imara za mfumo wa Kiislamu hapa nchini ni kuwa na moyo wa kishujaa na kusimama kwake kidete mbele ya makeke na upayukaji wa madola ya kibeberu. Aidha alisema kuwa, moja ya hila na ujanja unaotumiwa na madola vamizi ni kuyatisha mataifa na tawala za nchi nyingine na kutumia woga wa mataifa hayo kufanikisha malengo haramu ya madola hayo ya kibeberu na ndio maana mara zote utayaona madola hayo ya kiistikbari yakipenda kujigamba na kujionesha kuwa yana nguvu kubwa.
Kiongozi Muadhamu amesema bayana kwamba, kama Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran lingeyaogopa madola ya kibeberu na kulegeza kamba mbele yao, basi leo hii kusingekuwa na athari yoyote ile ya Iran na Uirani. Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, adui yeyote yule, awe Mmarekani au mkubwa kuliko Marekani hawezi kufanya lolote mbele ya mfumo wa utawala unaotegemea vizuri nguvu za wananchi wake na ambao umesimama kidete mbele ya adui.

No comments:

Post a Comment