Polisi nchini Zambia imemtia mbaroni Hakainde
Hichilema, kinara wa chama kikuu cha upinzani cha United Party for
National Development.
Stephen Katuka, Katibu Mkuu wa chama cha upinzani cha UPND
ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, maafisa wa polisi walivamia
makazi ya Hichilema na kumtia mbaroni bila kutoa maelezo yoyote kwa
familia yake.
Katuka amekosoa vikali hatua ya polisi kumtia nguvuni kinara wa
upinzani bila kutoa ufafanuzi wowote huku akitaja kama kitendo cha
kinyama hatua ya polisi kuvamia makazi ya mwanasiasa huyo bila waranti
na kisha kurusha mabomu ya kutoa machozi katika nyumba iliyokuwa na
watoto wadogo.
Hata hivyo baadhi ya duru za usalama zimedokeza kuwa, Hichilema
amekatwa kwa kuwa mwishoni mwa wiki alizuia msafara wa magari ya
Rais Edgar Lungu, magharibi mwa nchi.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, Oktoba mwaka jana, polisi ya Zambia
iliwatia mbaroni Hichilema na Geoffrey Mwamba, Mkuu na Naibu Mkuu wa
chama kikuu cha upinzani cha United Party for National Development kwa
tuhuma za uchochezi.
Uchaguzi wa Rais uliofanyika mwezi Agosti mwaka jana huko Zambia
ulikuwa wenye ushindani mkali kati ya Rais wa sasa wa nchi hiyo Edgar
Lungu na mgombea wa upinzani Hakainde Hichilema ambaye alidai kuibiwa
kura.
No comments:
Post a Comment