Saudi Arabia inafanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi na Sudan yajulikanayo kama
'Ngao ya Samawati -1' huku nchi hizo mbili zikijaribu kuimarisha uhusiano wao kutokana na vizingiti vya ndani ya nchi na kieneo.
Mazoezi hayo ya anga baina ya majeshi ya Sudan na Saudia
yanayofanyika katika mipaka ya kaskazini mwa Sudan, yameanza Machi 29 na
yataendelea hadi Aprili 12.
Uhusiano wa Sudan na Saudi Arabia umekuwa ukiimarika katika kipindi
cha mwaka mmoja uliopita. Sudan ni kati ya nchi ambazo zinashiriki
katika hujuma ya kinyama ya Saudia nchini Yemen. Pamoja na hayo,
ushiriki wa Sudan katika muungano huo wa Saudia, sawa na ushiriki wa
nchi zinginezo, ni wa kinembo tu na kwa ajili ya kupata misaada ya
kifedha ya Saudia.
Katika miezi ya hivi karibuni, maafisa wa Sudan na Saudia wamekuwa
wakikutana kujadili uhusiano wa pande mbili katika sekta za kisiasa,
kiuchumi na kijeshi.
Ingawa Sudan inataka misaada ya kifedha katika uhusiano wake na
Saudia, lakini mkondo wa kuimarika uhusiano wao ni katika fremu ya Saudi
Arabia kutaka kujipenyeza na kuwa na ushawishi barani Afrika. Ni kwa
msingi huo ndio maana Rais Omar El Bashir wa Sudan hivi karibuni akatoa
matamshi ya kustaajabisha kuwa eti usalama wa Saudia ni usalama wa
Sudan!
Sababu kuu ya Saudia kukodolea macho ya tamaa nchi za Afrika ikiwemo
Sudan ni matukio ya kasi Mashariki ya Kati ambayo hayaendi tena kwa
maslahi ya watawala wa Riyadh. Wakuu wa Saudia wanaamini kuwa, hivi sasa
uwezo na satwa yao iko katika mkondo wa kuporomoka katika eneo la
Mashariki ya Kati.
Kwa msingi huo, Saudia sasa inataka kutumia uwezo wake wa kifedha
ili kueneza ushawishi wake ya kisiasa barani Afrika na kupata waitifaki
katika bara hilo. Kwa msingi huo, Sudan imesema Saudia itawekeza dola
bilioni 111 nchini Sudan na kwamba kiwango hicho cha uwekezaji
kitaongozeka maradufu katika siku za usoni.
Wakati huo huo, Saudi Arabia kwa kufanya mazoezi ya kijeshi katika
nchi za Kiarabu na Kiafrika inataka kutuma ujumbe huu kwa nchi zingine
kuwa ina ushawishi mkubwa katika katika nchi za Kiafrika na Kiarabu.
Weledi wa mambo wanasema hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa Saudia
kufanya mazoezi ya kijeshi na Sudan, wakuu wa Riyadh wanataka kutuma
ujumbe kwa nchi jirani ya Misri. Hii ni kwa sababu mazoezi hayo
yanafanyika karibu na mpaka wa Sudan na Misri wakati uhusiano wa Misri
na Saudia unaripotiwa kuvurugika katika kipindi cha mwaka mmoja
uliopita.
Nukta muhimu hapa ni kuwa, licha ya mazoezi hayo ya kijeshi, uhusiano
wa Sudan na Saudia unaimarika kwa sababu ya matatizo yaliyoibuka hivi
sasa katika nchi hizo mbili. Katika upande mmoja Saudia inashuhudia
kufeli sera zake zisizo na busara Mashariki ya Kati huku serikali ya
Omar El Bashir nayo ikikumbwa na matatizo mengie ya kiuchumi na hivyo
kuwa chini ya mashinikizo makubwa ya wananchi.
No comments:
Post a Comment