Mahakama ya Juu nchini India imetoa hukumu
kwamba wanasiasa wa chama tawala nchini humo cha Bharatiya Janata Party
(BJP) wanapaswa kupandishwa kizimbani kwa kuhusika na kitendo cha
kubomolewa msikiti wa kihistoria nchini humo.
Wakitoa uamuzi hii leo, majaji wa
mahakama hiyo wamesema Uma Bharti, waziri wa maji, L K Advani, Naibu
Waziri Mkuu wa zamani pamoja na mwanasiasa mashuhuri M M Joshi, wote hao
wa chama tawala BJP wanapaswa kufunguliwa mashtaka ya jinai na kula
njama, kwa kuwachochea vijana wenye misimamo mikali wa Kihindu kuubomoa
Msikiti wa Babri wa karne ya 16, mwaka 1992.
Kadhalika Mahakama ya Juu ya India
imepitisha kuwa, mwanasiasa mwingine mkongwe wa chama tawala nchini
humo, Kalyan Singh anafaa kufunguliwa mashtaka pamoja na wenzake watatu
kuhusiana na kadhia hiyo, kwa kuwa wakati wa ubomoaji wa msikiti huo wa
kale, alikuwa mkuu wa Jimbo la Uttar Pradesh.
Sanjay Jha, Msemaji wa Muungano wa
Upinzani nchini humo amepongeza uamuzi huo uliotolewa leo Jumatano na
Mahakama ya Juu ya India, akisisitiza kuwa, korti imeonelea kwamba kuna
ushahidi wa kutosha wa kuwapandisha kizimbani wanasiasa hao wa chama
tawala.
Baada ya kubomolewa Msikiti wa Babri
katika mji wa Ayodhya, Jimbo la Uttar Pradesh, kaskazini mwa India
tarehe 6 Disemba 1992, machafuko yalitawala eneo hilo, ambapo maelfu ya
watu waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.
No comments:
Post a Comment