Wednesday, April 19, 2017

WANASIASA WA CHAMA TAWALA INDIA KIZIMBANI KWA KUCHOCHEA KUBOMOLEWA MSIKITI

Mahakama ya Juu nchini India imetoa hukumu kwamba wanasiasa wa chama tawala nchini humo cha Bharatiya Janata Party (BJP) wanapaswa kupandishwa kizimbani kwa kuhusika na kitendo cha kubomolewa msikiti wa kihistoria nchini humo.
Wakitoa uamuzi hii leo, majaji wa mahakama hiyo wamesema Uma Bharti, waziri wa maji, L K Advani, Naibu Waziri Mkuu wa zamani pamoja na mwanasiasa mashuhuri M M Joshi, wote hao wa chama tawala BJP wanapaswa kufunguliwa mashtaka ya jinai na kula njama, kwa kuwachochea vijana wenye misimamo mikali wa Kihindu kuubomoa Msikiti wa Babri wa karne ya 16, mwaka 1992.
Kadhalika Mahakama ya Juu ya India imepitisha kuwa, mwanasiasa mwingine mkongwe wa chama tawala nchini humo, Kalyan Singh anafaa kufunguliwa mashtaka pamoja na wenzake watatu kuhusiana na kadhia hiyo, kwa kuwa wakati wa ubomoaji wa msikiti huo wa kale, alikuwa mkuu wa Jimbo la Uttar Pradesh.
Vijana wenye misimamo mikali wa Kibaniani wakishangilia baada ya kubomoa msikiti wa kale Babri nchini India
Sanjay Jha, Msemaji wa Muungano wa Upinzani nchini humo amepongeza uamuzi huo uliotolewa leo Jumatano na Mahakama ya Juu ya India, akisisitiza kuwa, korti imeonelea kwamba kuna ushahidi wa kutosha wa kuwapandisha kizimbani wanasiasa hao wa chama tawala.
Baada ya kubomolewa Msikiti wa Babri katika mji wa Ayodhya, Jimbo la Uttar Pradesh, kaskazini mwa India tarehe 6 Disemba 1992, machafuko yalitawala eneo hilo, ambapo maelfu ya watu waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

No comments:

Post a Comment