Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC)
imetahadharisha kuwa ukatili uliofanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Congo ikiwa ni pamoja na mauaji ya wataalamu wawili wa Umoja wa
Mataifa unaweza kutambuliwa kuwa ni jinai ya kivita.
Taarifa hiyo ya mahakama ya ICC imetolewa baada ya mauaji ya
karibu watu 400 wakiwemo wataalamu wawili wa Umoja wa Mataifa raia wa
Marekani na Sweden katika mkoa wa katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Congo wa Kasai.
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai Fatou
Bensouda amesema kuwa, amepokea ripoti kuhusu ukatili unaofanyika katika
mapigano yamayojiri kati ya makundi ya wanamgambo na jeshi la serikali
ya Congo, mauaji ya idadi kubwa ya raia, utekaji nyara na kunyongwa ovyo
watu wasio na hatia. Amesisitiza kuwa vitendo hivyo vinaweza
kutambuliwa kuwa ni jinai za kivita.
Bensouda amesisitiza kuwa hatasita kuwachukulia hatua na kuwapandisha kizimbani watu wanaohusika na uhalifu huo.
Mkoa wa Kasai umekumbwa na ghasia tangu katikati ya mwezi Agosti,
wakati askari wa kikosi cha serikali ya Congo walipomuua Kamwina Nsapu,
aliyekuwa kiongozi wa wanamgambo waasi dhidi serikali kuu Rais Joseph
Kabila.
Wiki iliyopita pia wanamgambo wa eneo hilo waliwaua kwa kuwakata
vichwa maafisa karibu 40 wa jeshi la polisi ya nchi hiyo katika maeneo
ya msituni mkoani Kasai.
No comments:
Post a Comment