Russia na China zimetuma meli zao za kijeshi
katika eneo zilipo meli za Marekani karibu na pwani ya Korea Kaskazini
kwa lengo la kufuatilia nyendo za meli za Marekani katika eneo hilo.
Gazeti la Japan la Yomiuri Shimbun
limeandika kuwa, serikali ya Uchina imeomba msaada kwa Russia kwa ajili
ya kuzuia kutokea mgogoro wa kivita huko Korea Kaskazini. Kwa mujibu wa
gazeti hilo, Beijinga na Moscow zimeamua kutuma meli zao za kivita kwa
ajili ya kukusanya taarifa za kiintelijensia kutoka meli za Marekani,
ili kuzuia kuongezeka kwa mgogoro baina ya Marekani na Korea Kaskazini.
Wakati huo huo gazeti la Japan News,
linaloandikwa kwa lugha ya Kingereza limesema kuwa, meli hizo za Uchina
na Russia zitakuwa na kazi ya kutoa indhari na kupiga doria sambamba na
kuzidisha ulinzi wa kujitawala anga na bahari ya eneo hilo. Awali Rais
Donald Trump wa Marekani alitoa amri ya kutumwa meli tatu za kubeba
ndege za kivita za 'USS Carl Vinson' 'Ronald Reagan' na 'USS Nimitz'
kwenda pwani ya Korea, hatua ambayo ilitajwa na serikali ya Pyongyang
kuwa ni ya kichokozi.
Katika hatua nyingine serikali ya Korea Kusini imesisitiza azma yake
ya kuweka ngao ya makombora ya Marekani aina ya THAAD katika ardhi yake
na kwamba hakuna mabadiliko yoyote katika suala hilo. Wizara ya Ulinzi
ya nchi hiyo ilisema Jumatatu ya jana katika kujibu baadhi ya tetesi
zilizoashiria kuwa Seoul na Washington zimeamua kusitisha zoezi la
uwekaji ngao hiyo, kwamba habari hizo hazina ukweli wowote.
No comments:
Post a Comment