Danny Danon Balozi wa Utawala wa Kizayuni katika Umoja wa Mataifa amekosoa vikali matamshi ya katibu mkuu wa umoja huo Antonio Gutterres ambaye ameunga mkono uundwaji nchi huru ya Palestina.
Dannon amesema Umoja wa Mataifa unapaswa kujizuia kueneza kile alichodai kuwa ni urongo na kuangazia uhalisia wa mambo katika eneo.
Mjumbe huyo wa utawala wa Kizayuni amedai kuwa ni kichekesho kutuhumiwa kwa ugaidi utawala pekee wa kidemokrasia katika eneo.
Madai hayo ya Dannon kuwa eti utawala wa Kizayuni wa Israel ndio "utawala pekee wa kidemokrasia" Mashariki ya Kati na jitihada za utawala huo za kupotosha ukweli katika eneo hili zinajiri wakati ambao utawala huo umezidisha sera zake za uvamizi na utumiaji mabavu katika eneo. Hivi sasa utawala haramu wa Israel unatambulika kimataifa katika dhihirisho la ukaliaji mabavu, mienendo iliyo dhidi ya binadamu na ubaguzi. Sera hizo za Israel zimezua radiamali za kimataifa.
Kuhusiana na hilo Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jumanne alitaka kuundwe nchi huru ya Palestina na kusema hilo limekuwa takwa la walimwengu kwa muda wa miaka 70 sasa.
Guterres alikuwa akizungumza kwa munasaba wa mwaka wa 50 wa maafa ya 1967 ya kukaliwa kwa mabavu ardhi zaidi za Palestina. Katika taarifa aliyotoa kwa munasaba huo, Gutteres ameitaka Israel ihitimishe ukaliaji wake wa mabavu wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Quds Mashariki na Miinuko ya Golan.
Aidha amesisitiza kuwa, kadhia ya Palestina na Wazayuni inapaswa kutatuliwa kwa msingi wa maazimio ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.
Utawala wa Kizayuni umekasirishwa na kauli ya Guterres katika hali ambayo ukatili wa utawala huo ghasibu umesajiliwa katika nyaraka za Umoja wa Mataifa na walimwengu hawatasahau ukatili huo wa Wazayuni.
Utawala wa Kizayuni ni utawala haramu ambao unaungwa mkono na madola ya Magharibi na uliasisiwa mwaka 1948 kwa lengo la kutekeleza sera za kigaidi dhidi ya Wapalestina na kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina ikiwa ni pamoja na Quds Tukufu. Kwa hivyo tokea kuasisiwa kwake, utawala huo umekuwa ni utawala wa shari na vamizi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Katika fremu hiyo katika vita vya mwaka 1967, utawala wa Kizayuni katika vita vyake na nchi za Kiarabu ulikalia kwa mabavu ardhi zaidi za Palestina ikiwa ni pamoja na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na sehemu ya Baitul Maqqdis na sehemu ya ardhi za nchi za Kiarabu ikiwa ni pamoja na Miinuko ya Golan ya Syria. Kwa hivyo utambulisho wa kivita wa utawala huo uko wazi kwa walimwengu.
Utawala huo umekuwa ukijaribu kubadilisha fikra za walimwengu kwa kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya taasisi za kimataifa.
Maazimio kadhaa ya taasisi za kimataifa hasa Umoja wa Mataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel hasa kulaani sera za ukaliaji mabavu za utawala huo ni jambo linaloonyesha kuwa jamii ya kimataifa haikubali sera za kujitanua za utawala huo.
Matukio ya kimataifa yanaonyesha jamii ya kimataifa haiwezi kustahamili tena kushuhudia jinai za utawala huo wa Kizayuni ambao ni utawala haramu na ambao unapata himaya ya nchi za Magharibi.
Maazimio mbali mbali ya Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na azimio 242 na 338 yamebainisha wazi kuwa utawala wa Kizayuni unapaswa kuondoka katika ardhi unaozikalia kwa mabavu.
Katika miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa harakati za kimataifa za kuunga mkono haki za watu wa Palestina ikiwa ni pamoja na kuinua hadhi ya Palestina katika Umoja wa Mataifa.
Aghalabu ya nchi za dunia zinaunga mkono kuundwa nchi huru ya Palestina mji wake mkuu ukiwa ni Quds Tukufu na kuna uwezekano kuwa mwaka huu wa 2017 nchi huru ya Palestina itaundwa
Mchakato huu umeutia wasi wasi utawala haramu wa Israel na ndio sababu wakuu wa utawala huo wameanza kutoa matamshi dhidi ya Umoja wa Mataifa kutokana na sisitizo la umoja huo kuhusu ulazima wa utawala huo wa Kizayuni kusitisha ukaliaji mabavu ili taifa huru la Palestina liundwe.
No comments:
Post a Comment