Mbunge katika chama tawala cha Republican nchini Marekani amesema hujuma za hivi karibuni za kundi la kigaidi la ISIS mjini Tehran inaweza kuwa stratijia ya Rais Donald Trump.
Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Dana Rohrabacher, ambaye anawakilisha California katika Bunge la Kongresi, ametoa matamshi hayo katika kikao cha Alhamisi cha Kamati ya Sera za Kigeni ya Kongresi ambayo ilikuwa ikijadili kuhusu Harakati ya Hizbullah ya Lebanon.
Dana Rohrabacher ambaye alionekana kuunga mkono hujuma za kigaidi za Jumatano dhidi ya watu wa Iran alisema kundi la kigaidi lililotekeleza hujuma hiyo linapaswa kuchochewa zaidi kuishambulia Iran.
Ikumbukwe kuwa siku ya Jumatano, timu ya magaidi wa Daesh (ISIS) walishambulia Haram ya Imam Khomeini MA na eneo la Bunge la Iran mjini Tehran na kuwaua shahidi watu 17 huku wengine karibu 50 wakijeruhiwa. Magaidi watano waliotekeleza hujuma hiyo waliangamizwa na maafisa wa usalama huku wahusika wengine 41 wakikamatwa katika maeneo mbali mbali ya Iran.
Mbunge huyo mwenye misimamo mikali wa chama cha Republican amesema iwapo stratijia ya Trump ni kuchochea hujuma za kigaidi Iran basi anaunga mkono jambo hilo. Amesema anaunga mkono Marekani kushirikiana na ISIS katika vita dhidi ya Iran na kutoa mfano wa namna Marekani ilivyoshirikiana na Joseph Stalin, aliyemtaja kuwa muovu, katika kumuangusha Adolf Hitler katika Ujerumani ya Wanazi.
Ifahamike kuwa kundi la ISIS lilianzishwa miaka kadhaa iliyopita kwa uungaji mkono wa kifedha na kijeshi wa Marekani na waitifaki wake wa Kiarabu hasa Saudi Arabia. Kundi hilo limetenda jinai za kuogofya katika nchi kadhaa hasa Iraq na Syria lakini katika miezi ya hivi karibuni limeanza kupata pigo na kupoteza ardhi ambazo lilikuwa limeziteka katika nchi hizo mbili.
No comments:
Post a Comment