Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, matukio yanayojiri nchini Yemen na Bahrain ni jeraha kubwa linaoukabili umma wa Kiislamu na ameutaka ulimwengu wa Kiislamu kulisaidia kwa hali na mali taifa ya Yemen.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo asubuhi katika hotuba aliyoitoa baada ya swala ya Iddil-Fitri iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran ambapo ameutaka umma wa Kiislamu kusimama imara na kuisaidia Yemen kwa namna ya wazi kabisa kutokana na ukatili inaofanyiwa. Amesisitiza kwa kusema: "Ni lazima maulamaa wa Kiislamu wachukue hatua kuhusiana na kinachojiri katika baadhi ya nchi za Kiislamu hata kama suala hilo litawakasirisha makafiri."
Kadhalika amezungumzia mafanikio mbalimbali ya kimaanawi yaliyopatikana ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani uliomalizika jana Jumapili, yakiwemo matendo ya ibada na kusema kuwa, shambulio la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran SEPAH dhidi ya magaidi katika mji wa Deir Ezzor nchini Syria, ni amali tukufu ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kushiriki kwa wingi watu katika matembezi ya siku hiyo tukufu ni miongoni mwa matukio muhimu yaliyotokea ndani ya mwezi humo mtukufu wa Ramadhani. Swala ya Iddul-Fitri nchini Iran imeswalishwa kitaifa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei hapa Tehran, ambapo idadi kubwa ya Waislamu wa mji wa Tehran wameshiriki swala hiyo.
Ni zaidi ya miaka mitatu sasa ambapo taifa la Yemen linashuhudia mashambulizi makali na mzingiro wa kila upande wa Saudia na washirika wake wa nchi Kiarabu kwa baraka kamili za Marekani, Israel na baadhi ya nchi za Ulaya.
No comments:
Post a Comment