Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh wanawapiga risasi watoto wanaokimbia vita na mapigano katika mji wa Mosul huko kaskazini mwa Iraq.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa imetahadharisha kuwa, mauaji yanayofanywa na kundi la Daesh dhidi ya raia wanaokimbia mapigano katika mji wa Mosul yamekifikia kiwango cha kutia wasiwasi.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, katika siku chache zilizopita tu raia 231 waliokuwa wakikimbia mapigano huko Mosul wameuawa kwa kupigwa risasi na wapiganaji wa Daesh.
Taarifa ya Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa pia imesema mauaji ya raia yanayosababishwa na mashambulizi ya anga yanatia wasiwasi. Mashambulizi hayo yanafanywa na Marekani na washirika wake.
Wakati huo huo mjumbe wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) nchini Iraq amesema kuwa inakadiriwa kuwa, zaidi ya Wairaq laki moja wanasumbuliwa na hali mbaya kupita kiasi katika mji wa Mosul.
Jeshi la Iraq linaendeleza operesheni ya kukomboa mji huo kutoka kwenye makucha ya kundi la kigaidi la Daesh. Operesheni hiyo ilianza tarehe 19 Februari mwaka huu.
No comments:
Post a Comment