Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kitendo cha Marekani cha kuzusha vurugu mpya nchini Syria kwa kutegemea madai ya uongo, si kwa faida ya yeyote isipokuwa magaidi wa ISIS.
Itakumbukwa kuwa, mapema leo alfajiri, Sean Spicer, msemaji wa Ikulu ya Marekani (White House) amedai bila ya ushahidi wowote kwamba, iwapo Syria itafanya shambulio la kemikali, basi italazimika kutoa gharama kubwa ya shambulio hilo.
Shirika la habari la IRIB limemnukuu Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran akisema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Tweeter kwamba, njama za Marekani za kuzusha vurugu mpya nchini Syria kwa madai ya uongo ni kwa manufaa ya magaidi wa Daesh tu tena katika wakati huu ambapo genge hilo linazidi kuangamizwa na wananchi wa Iraq na Syria.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha amesema kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu ya Marekani wa kuruhusu kutekelezwa siasa za rais wa Marekani, Donald Trump za kupiga marufuku raia wa nchi za Kiislamu kuingia nchini Marekani, hauwezi kuidhaminia Marekani usalama wake. Pia amesema, inachotakiwa kufanya Marekani ni kuachana na siasa za misimamo mikali na kujiunga na wale wanaopambana kikweli na misimamo hiyo.
Jana Jumatatu, Mahakama Kuu ya Marekani iliiruhusu serikali ya Donald Trump itekeleze marufuku yake ya siku 90 ya kuingia nchini Marekani raia wa nchi za Kiislamu za Iran, Libya, Somalia, Sudan, Syria na Yemen. Katika miezi ya Januari na Machi 2017, Trump alitoa amri ya kuzuiwa kuingia Marekani raia wa nchi hizo sita za Kiislamu. Hata hivyo hadi hivi sasa amri hiyo ilikuwa imekwama kutokana na majimbo mbalimbali ya Marekani kukataa kuitekeleza.
No comments:
Post a Comment