Wednesday, June 7, 2017

MAGAIDI WASHAMBULIA BUNGE LA IRAN NA HARAM YA IMAM KHOMEINI

Watu wawili akiwemo afisa wa usalama wameripotiwa kuuawa huku watu wengine wanane wakijeruhiwa baada ya watu waliojizatiti kwa silaha kushambulia majengo ya Bunge la Iran na Haram ya Imam Khomeini MA, katika mji mkuu Tehran.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, watu wanne waliokuwa wamejizatiti kwa bunduki za AK47 na bunduki moja ndogo wamefyatua risasi ovyo wakilenga walinzi wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ambapo mlinzi mmoja ameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa.
Hata hivyo shirika la habari la ISNA limenukuu mbunge mmoja wa Tehran, Elias Hazrati  akisema kuwa hali hiyo imedhibitiwa na mvamizi mmoja ametiwa mbaroni.
Haram ya Imam Khomeini MA
Wakati huohuo, shirika la habari la Fars limeripoti kuwa, mtu mmoja ameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa baada ya watu watatu waliobeba silaha kuvamia Haram ya Imam Khomeini MA, viungani mwa Tehran. Mmoja wa wavamizi hao ameuawa na maafisa usalama, mwingine ambaye anasemekana kuwa mwanamke amejiripua huku wa tatu akijeruhiwa na kukamatwa na vyombo vya usalama.
Duru za kiusalama zimeripoti kuwa, fulana lililosheheni mada za miripuko la wavamizi hao katika Haram ya Imam Khomeini MA limepatikana na kuharibiwa.
Genge la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) limetangaza kuhusika na mashambulizi hayo ya leo jijini Tehran.

No comments:

Post a Comment