Msemaji wa serikali ya Tunisia ametangaza
habari ya kukamatwa mamia ya matakfiri wanaorejea nchini humo kutoka
eneo la Mashariki ya Kati.
Iyad Dahmani, msemaji wa serikali hiyo amesema kuwa tokea mwaka
2007 hadi sasa matakfiri wapatao 800 wa Kitunisia wametiwa mbaroni na
kufungwa jela baada ya kurejea nchini humo kutokea Syria, Iraq na Libya
na kwamba hivi sasa wako chini ya uangalizi mkali. Akizungumzia suala
hilo hivi karibuni, Youssef Chahed, Waziri Mkuu wa Tunisia amesema kuwa
serikali yake haijatia saini mkataba wowote wa kurejeshwa nchini humo
magaidi wa kitakfiri na kwamba serikali hiyo haiungi mkono kurejea
nchini humo kwa magaidi hao.
Wiki iliyopita, Hadi Majdub, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tunisia
alitangaza habari ya kurejkea nchini matakfiri 800 na kuongeza kuwa
viongozi wa nchi hiyo wana habari kamili kuhusiana na magaidi hao. Tokea
kuanza kwa vita huko Syria maelfu ya Watunisia waliamua kujiunga na
kundi la kigaidi la Daesh na kushiriki katika vitendo vya kinyama na
kigaidi dhidi ya wananchi wa Syria. Hata hivyo katika miezi ya hivi
karibuni ambapo kundi hilo limekuwa likidhoofika siku baada ya siku
kufuatia kushindwa katika medani za vita katika nchi hiyo na Iraq,
wanachama wa Daesh wamekuwa wakitafuta njia za kurudi katika nchi zao,
jambo ambalo limewatia wasiwasi mkubwa viongozi wa nchi hizo na hasa wa
Tunisia.
No comments:
Post a Comment