Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi
Rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi amesema
kuwa, huenda akagombea tena urais kwa kipindi cha nne mfululizo kama
wananchi wa Burundi watamtaka kufanya hivyo.
Nkurunziza ambaye uamuzi wake wa
kugombea urais kwa kipindi cha tatu mfululizo umeitumbukiza Burundi
kwenye mgogoro mkubwa amesema katika mkutano mmoja uliofanyika mjini
Rutuna, kusini mashariki mwa Burundi kwamba: "Kwa vile tunaheshimu
utawala wa sheria na iwapo wananchi watapitisha kuwa, kugombea tena si
kuvunja sheria, na kama wananchi wataomba jambo hilo, hatuwezi kusaliti
imani ya nchi, hatuwezi kusaliti imani ya wananchi.
Aidha amesema, kuna uwezekano katiba ya
Burundi ikafanyiwa marekebisho na kuondoa kipengee cha ukomo wa kugombea
urais nchini humo na pia kipindi cha miaka mitano uongozini.
Wakati aliposhiriki kwenye uchaguzi kwa
mara ya tatu mfulilizo mwaka 2015, Nkurunziza alidai kuwa kuchaguliwa
kwake kwa mara ya kwanza mwaka 2005 kulikuwa kwa kipindi cha mpito baada
ya vita vya ndani hivyo alikuwa na haki ya kugombea urais kwa mara ya
tatu.
Hata hivyo wapinzani waliilalamikia
vikali hatua hiyo na kusema kuwa ni kinyume na makubaliano ya Arusha
Tanzania yanayompa haki mtu kuongoza Burundi kwa vipindi viwili.
Tangu wakati huo hadi hivi sasa Burundi
imeshuhudia machafuko mengi, huku wataalamu wa Umoja wa Mataifa
wakiripoti kutokea kesi chungu za uvunjaji wa haki za binadamu, mateso,
udhalilishaji wa kijinsia, kutiwa mbaroni watu kwa umati na kupotezwa
bila kujulikana waliko.
Burundi ina historia ndefu ya machafuko
baina ya makabila ya Kihutu na Kitutsi yaliyopelekea nchi hiyo ndogo ya
katikati mwa Afrika kushuhudi miaka 12 ya mapigano ya ndani yaliyoanza
mwaka 1993 na kumalizika 2006 kwa mujibu wa Makubaliano ya Arusha.
No comments:
Post a Comment