Duru za Yemen zimeripoti kuwa, ndege moja ya
Uturuki imewahamishia nchini humo makumi ya magaidi wa Daesh (ISIS) kwa
kutumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aden, kusini mwa Yemen, baada ya
magaidi hao kufurushwa nchini Syria.
Mtandao wa habari wa al Masirah wa
Yemen umeripoti kuwa, ndege ya Uturuki iliyokuwa na magaidi 150
waliofurushwa katika mji wa Halab (Aleppo) wa kaskazini magharibi mwa
Syria, imetua katika uwanja huo, ikiwa ni uingiliaji wa wazi wa masuala
ya ndani ya Yemen. Tarehe 22 Disemba mwaka huu, jeshi la Syria
lilitangaza kukombolewa kikamilifu mji wa Halab baada ya magaidi wote
kuukimbia mji huo baada ya kuukalia kwa zaidi ya miaka minne.
Duru za usalama za Yemen zimetangaza
kuwa, ndege ya Uturuki iliyowabeba magaidi hao iliongozwa na vikosi
vamizi ya Umoja wa Falme za Kiarabu ambavyo vinashiriki katika
mashambulizi ya kivamizi yanayoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya wananchi
wa Yemen.
Vile vile mtandao wa habari wa al
Masirah umesema kuwa, ndege hiyo ya Uturuki itabeba mamluki 158 wa Saudi
Arabia waliojeruhiwa na wanajeshi na vikosi vya wananchi wa Yemen
katika mkoa wa Ta'izz. Majeruhi hao watatibiwa katika hospitali za
Uturuki. Uturuki inatajwa kuwa moja ya waungaji mkono wakuu wa magenge
ya kigaidi nchini Syria kama ambavyo pia inalaumiwa kwa kutoa mafunzo
kwa magenge ya kigaidi yanayofanya jinai ndani ya Syria.
Hadi sasa mashambulizi ya kivamizi
yanayoongozwa na Saudi Arabia huko Yemen yameshaua watu zaidi ya 11,400,
kwa mujibu wa kundi la haki za binadamu lisilo la kiserikali la Yemen
lijulikanalo kwa jina la Kituo cha Kisheria kwa Ajili ya Haki za
Binadamu na Maendeleo
No comments:
Post a Comment