Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
amewataka viongozi wa nchi zote duniani kuimarisha umoja na mshikamano
na kujiepusha na hitilafu na mifarakano.
Jan Eliasson mbaye muda wake wa kuhudumu katika cheo hicho
unamalizika kesho sambamba na kumalizika mwaka huu wa 2016 amesema umoja
na mshikamano ndiyo haja kubwa zaidi ya dunia ya sasa na kuongeza kuwa,
kuna haja ya kutafakari na kutafuta njia ya kutatua migogoro ya dunia
kama suala la wahamiaji, wakimbizi na kusitishwa vita katika maeneo
mbalimbali.
Eliasson pia amewataka viongozi wa nchi mbalimbali kuacha tabia ya
kusisitiza juu ya migawanyiko ya kiutaifa, kikabila au kidini. Adha
amesisitiza umuhimu wa kuheshimiwa haki za binadamu.
Kuhusu suala lililomkatisha tamaa zaidi kama Naibu Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson amesema ni maafa ya Syria na kwamba
Umoja wa Mataifa umeshindwa kukomesha mgogoro huo.
Amesema mgogoro wa Syria umesasababisha mauaji ya mamia ya maelfu ya
binadamu na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi katika
nchi nyingine. Amesisitiza kuwa mgogoro wa Syria umesababisha ukosefu wa
uthabiti katika siasa za kimataifa.
No comments:
Post a Comment