Duru za Palestina zimetangaza kuwa, utawala
wa Kizayuni wa Israel umechimba mashimo mapya chini ya Msikiti wa al
Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Habari hiyo imetangazwa na Kamati ya Kiislamu na Kikristo kwa
Ajili ya Kulinda Quds na Matukufu yake. Katibu Mkuu wa kamati hiyo Dk,
Hanna Issa ametahadharisha juu ya hatari ya mashimo hayo ya chini ya
ardhi kwa majengo na taasisi za Msikiti wa Al-Aqsa na kueleza kwamba,
idadi ya mashimo hayo ya chini kwa chini katika mji wa Quds ambayo
yanaviunganisha pamoja vitongoji wa walowezi wa Kizayuni yamefikia 27.
Tangu utawala wa Kizayuni wa Israeli ulipouvamia na kuanza kuukalia
kwa mabavu mji wa Quds mwaka 1967 hadi sasa unaendelea kuchimba mashimo
ya chini ya ardhi katika mji huo hasa katika eneo lake la kale na
kandokando mwa Msikiti wa Al-Aqsa ili kuwalazimisha Wapalestina wayahame
maeneo hayo na kuweza kuyadhibiti maeneo yanayozunguka msikiti huo. Ili
kuharakisha zoezi la kufikiwa lengo hilo na kuvunja Msikiti wa al Aqsa
ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu, utawala huo ghasibu umekuwa
ukichimba mashimo chini ya eneo hilo takatifu na kandokando yake kwa
shabaha ya kudhoofisha msingi na nguzo zake. Suala hilo linahatarisha na
kuzidisha uwezekano wa msikiti huo kuporomoka na kuvunjika iwapo
kutatokea tetemeko dogo la ardhi na matukio mengine kama hayo. Vilevile
Israel inafanya mikakati ya kuanzisha tetemeko la makusudi la ardhi kwa
kulipua maeneo ya chini ya Msikiti wa al Aqsa, ili ionekane kwamba,
uharibifu wa msikiti huo umetokana na suala la kimaumbile. Kwa sababu
hiyo duru za kuaminika zinasema, njama na mipango ya utawala haramu wa
Israel ya kuvunja Msikiti wa al Aqsa imeingia katika awamu nyeti na
hatari sana.
Kwa miaka mingi sasa Israel imekuwa ikitekeleza mpango wa kubadilisha
utambulisho wa Kiislamu wa mji wa Quds tukufu kwa kuharibu turathi za
Kiislamu na za kale za mji huo na kuweka badala yake alama za Kiyahudi.
Katika mkondo huo Israel imekuwa ikiharibu misikiti, majumba ya
kihistoria, maeneo ya makaburi ya kale, vituo vya kiutamaduni, mashamba
na nyumba za Wapalestina na kujenga maabadi za Wayahudi na vitongoji vya
walowezi wa Kizayuni. Hayo yanafanyika licha ya kwamba maazimio nambari
242 na 338 ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na vilevile kifungu
nambari nne cha Mkataba wa Geneva vimepiga marufuku aina yoyote ya
ujenzi na kubadilisha utambulisho wa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya
Palestina.
Jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel kama zile za
kuharibu au kuvunjia heshima maeneo matakatifu ya Kiislamu au kuvamia
maeneo hayo na kuwafukuza Wapalestina ni kielelezo cha siasa za kibaguzi
za utawala huo dhidi ya wafuasi wa dini za mbinguni na uhuru wa
kuabudu. Kwa msingi huo kuna udharura kwa jumuiya za kimataifa kuchukua
msimamo mmoja na madhubuti wa kukabiliana kivitendo na siasa hizo za
kibaguzi za Israel na zisitosheke kutoa maazimio yasiyokuwa na dhamana
ya utekelezaji dhidi ya utawala huo.
No comments:
Post a Comment