Marekani kuuhamishia Quds (Jerusalem) ubalozi wake wa Tel Aviv mwezi Mei mwaka huu
Licha ya upinzani mkubwa ulioanzia eneo la
Mashariki ya Kati na ulimwengu kwa jumla, Wizara ya Mambo ya Nje ya
Marekani imetangaza kuwa mnamo mwezi Mei mwaka huu ubalozi wa nchi hiyo
ulioko Tel Aviv utahamishiwa Baitul Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu.
Heather Nauert, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani
ameeleza kupitia taarifa aliyotoa hapo jana kuwa ubalozi mpya wa nchi
hiyo huko Israel utafunguliwa katika mji wa Quds tarehe 14 Mei mwaka
huu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv
utahamishiwa mahali ulipo ubalozi mdogo wa nchi hiyo katika eneo la
Arnona kusini mwa mji wa Baitul Muqaddas.
Ikumbukwe kuwa tarehe 14 Mei, ambayo Marekani imepanga kuuhamishia
ubalozi wake katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu,
inasadifiana na maadhimisho ya mwaka wa 70 wa siku ulipoasisiwa utawala
haramu na bandia wa Kizayuni, ambayo Wapalestina wanaiita "Siku ya
Nakba". Katika siku hiyo wananchi madhulumu wa Palestina walihamishwa
kwa umati katika ardhi na makazi yao ya asili.
Waziri wa Intelijinsia wa utawala haramu wa Israel Yisrael Katz
amepongeza uamuzi huo uliotangazwa na Washington na kueleza kwa furaha
kuwa hakuna zawadi kubwa zaidi ya hiyo kwa utawala huo wa Kizayuni.
Itakumbukwa kuwa wakati Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence
alipohutubia bunge la Israel tarehe 22 ya mwezi uliopita wa Januari
alitangaza kwamba Washington inapanga kuuhamishia Quds ubalozi wake wa
Tel Aviv mnamo mwishoni mwa mwaka ujao wa 2019.
Tarehe 6 Desemba mwaka 2017, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza
kuwa Washington inaitambua rasmi Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa
utawala haramu wa Israel. Trump aidha alieleza azma yake ya kuuhamishia
kwenye mji huo ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv, suala ambalo
liliamsha hasira kubwa za wananchi wa Palestina na kulaaniwa pia kieneo
na kimataifa.
Sambamba na hayo mnamo tarehe 21 Desemba, Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa lilipitisha azimio lililoungwa mkono na nchi 128
wanachama ambalo lilisisitiza kuwa umoja huo hautoitambua Baitul
Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Mji wa Baitul Muqaddas ni mahali ulipo msikiti mtukufu wa Al Aqsa
ambao ni kibla cha mwanzo cha Waislamu na ni sehemu isiyotenganika na
ardhi ya Palestina na ni moja ya maeneo matatu makuu matakatifu ya
Kiislamu yenye hadhi na umuhimu maalumu mbele ya Waislamu.
Mji huo ulivamiwa na kuanza kukaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel mwaka 1967.../
No comments:
Post a Comment