Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania ameagiza
kusitishwa mara moja usajili wa meli mpya nchini humo kufuatia
kukamatwa dawa za kulevya na bidhaa nyingine zilizopigwa marufuku
kimataifa ndani ya meli zinazopeperusha bendera ya Tanzania.
Rais
Magufuli ametoa agizo hilo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano wa Tanzania, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Ujenzi,
Mawasiliano na Usafirishaji wa Zanzibar, Balozi Ali Abeid Karume
kufuatilia suala hilo mara moja. Kadhalika Magufuli amemuagiza Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine
Mahiga kusimamia utekelezaji wa agizo hilo na kuhakikisha kuwa jina la
Tanzania halichafuliwi ndani na nje ya nchi.
“Kafanyeni uchunguzi wa kina kwa meli
zote zinazopeperusha bendera ya Tanzania, fanyeni uchunguzi kwa meli
zilizokamatwa ambazo ni tano na pia hizi 470 zilizosajiliwa na
zinaendelea kufanya kazi zichunguzeni, hatuwezi kuacha jina la nchi yetu
lichafuliwe na watu wanaofanya mambo kwa masilahi yao.” Amesema Rais
Magufuli. Kadhalika amehimiza kutekelezwa kwa maagizo yaliyotolewa na
Makamu wa Rais Bi Samia Suluhu Hassan juzi, ambaye alitangaza kuzifutia
usajili meli mbili zilizokamatwa hivi karibuni sanjari na kuamuliwa
kushushwa bendera ya Tanzania kwenye meli hizo.
Suluhu alizitaja meli hizo kuwa ni
Kaluba iliyokamatwa maeneo ya Jamhuri ya Dominican Desemba 27 mwaka jana
ikiwa na wastani wa tani 1.6 ya dawa za kulevya pamoja na Andromeda
ambayo nayo iliyokamatwa ikisafirisha silaha kinyume cha sheria za
kimataifa. Matukio ya kukamatwa meli zenye mihadarati na zinazopeperusha
bendera ya Tanzania, yamekuwa yakiripotiwa nchi tofauti za dunia.
No comments:
Post a Comment