Watu watatu tu wameripotiwa kunusurika katika ajali ya ndege iliyochakaa aina ya Boeing 737 ambayo ilianguka hapo jana muda mfupi baada ya kuruka katika uwanja wa ndege wa Havana nchini Cuba huku wachunguzi wakijaribu kubaini chanzo cha ajali hiyo kupitia mabaki ya ndege hiyo.
Kwa mujibu wa televisheni ya taifa ya Cuba hali ya hewa ilikuwa ya mawingu na mvua ilikuwa inanyesha wakati ndege hiyo ambayo imeshatumika kwa muda wa miaka 39 ilipoanguka ikiwa katika safari za ndani kuelekea mji wa Holguin mashariki mwa nchi hiyo.
Rais Miguel Diaz-Canel wa Cuba amesema tume maalumu imeundwa kuchunguza chanzo cha ajali hiyo.
Ndege hiyo ilikuwa imebeba abiria 104, akthari yao wakiwa ni Wacuba pamoja na wahudumu sita.
Abiria wanne walionusurika walipelekwa hospitali ya Havana, ambapo hadi kufikia jana usiku watatu miongoni mwao walikuwa wangali hai.
Ajali hiyo ya jana ya ndege imetajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini Cuba katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita na ya tatu kwa ukubwa kutokea duniani tangu mwaka 2010.../
No comments:
Post a Comment