Watu sita wameuawa na wengine zaidi ya 20 wamejeruhiwa baada ya bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari kuripuka katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Meja Mohamed Hussein, afisa mwandamizi wa polisi nchini humo ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa bomu hilo limeripuka katika barabara yenye shughuli nyingi ya Makatul Mukaramah.
Amesema aghalabu ya wahanga wa hujuma hiyo inayoaminika kufanywa na kundi la kigaidi la al-Shabaab, ni wapita njia na watu waliokuwa ndani ya maduka yaliyoko kandokando ya barabara hiyo.
Afisa huyo wa polisi ya Somalia ameongeza kuwa, yumkini idadi ya vifo ikaongezeka, kutokana na majeraha mabaya waliyopata baadhi ya wahanga wa shambulizi hilo.
Wakati huohuo, makabiliano makali kati ya askari wa Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM na wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab yameripotiwa katika wilaya ya Bulamareer, eneo la Shabelle ya Chini, yapata kilomita 140 kusini magharibi mwa mji mkuu Mogadishu.
Hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na AMISOM au jeshi la Somalia kuhusu idadi ya wahanga wa mapigano hayo, ingawaje genge la al-Shabaab linadai kuwa limeua makumi ya askari wa Umoja wa Afrika.
AbdiAziz Abu Musab, msemaji wa operesheni za kijeshi za al-Shabaab amedai kuwa, kundi hilo la kigaidi limeua wanajeshi 39 wa AMISOM akiwemo kamanda wao.
No comments:
Post a Comment