Chuo Kikuu cha al Azhar cha nchini Miri kimeuonya utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na jinai unazozifanya pambizoni mwa Msikiti wa al Aqsa kwani jinai hizo zinawaumiza Waislamu wote duniani.
Chuo Kikuu cha al Azhar cha nchini Misri kilitoa tamko hilo jana Ijumaa huku taifa madhlumu la Palestina likiendelea kusimama kidete kukihami Kibla cha Kwanza cha Waislamu.
Katika tamko lake hilo al Azhar imeutaka ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu na taasisi za kieneo na kimataifa kuchukua hatua za haraka za kuuokoa Msikiti wa al Aqsa mbele ya jinai za utawala wa Kizayuni.
Tamko la chuo kikuu hicho cha Kiislamu cha nchini Misri limeongeza kuwa, al Azhar inalaani kwa nguvu zake zote uchochezi wote unaofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Waislamu wa Palestina waliokuwa wanasali na vile vile vitendo vya kikatili na kinyama vya Wazayuni ambavyo vimepelekea kujeruhiwa makumi ya Waislamu wa Palestina akiwemo khatibu wa Masjidul Aqswa, Sheikh Ekrima Sa'id Sabri.
Baada ya vijana watatu wa Kipalestina kufanya operesheni ya kujitolea kufa shahidi dhidi ya Wazayuni katika mji wa Quds siku ya Ijumaa ya tarehe 14 Julai, utawala wa Kizayuni wa Israel uliufunga msikiti huo na kuwazuia Waislamu kuingia msikitini humo kwa muda wa siku mbili.
Siku ya Jumapili, wanajeshi wa Israel walifungua milango ya msikiti huo lakini kwa masharti magumu ambayo Waislamu wa Palestina wameyapinga na kwa mara ya kwanza, jana Ijumaa, Wazayuni walizuia kusaliwa Sala ya Ijumaa ndani ya msikiti huo mtakatifu. Waislamu walimiminika katika maeneo ya karibu na msikiti huo kutekeleza ibada ya Sala ya Ijumaa, lakini hata hivyo hawakusalimika na ukatili wa Wazayuni.
Viongozi wengi wa nchi za Kiislamu na kimataifa wamelaani jinai hizo za Wazayuni na kuilaumu Israel kwa kutekeleza njama zake za muda mrefu dhidi ya Kibla cha Kwanza cha Waislamu kwa kutumia kisingizio cha opereseheni ya kujitolea kufa shahidi vijana hao watatu wa Palestina.
No comments:
Post a Comment